Jamii FM

Homera kuwa balozi ujenzi barabara ya Msimbati

28 October 2026, 14:03

Waziri wa Nishati Dkt. Juma Homera akizungumza na wananchi wa Msimbati waliojitokeza Oktoba 27, 2026 baada ya uzinduzi wa ugunduzi mpya wa gesi asilia katika kitalu cha Mnazi Bay (Picha na Musa Mtepa)

Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera, aahidi kupigania ujenzi wa barabara ya lami ya kilomita 35 kutoka Msimbati hadi Mtwara mjini ili wananchi wanufaike na rasilimali ya gesi asilia

Na Musa Mtepa

Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera, ameahidi kuwa mstari wa mbele katika kupigania ujenzi wa barabara ya kutoka Msimbati hadi Mtwara mjini kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa kilomita 35, ili kuwawezesha wananchi wa eneo hilo kunufaika na rasilimali ya gesi asilia inayozalishwa katika maeneo yao.

Akizungumza Oktoba 27, 2026, na wananchi wa Kata ya Msimbati, baada ya kuzindua ugunduzi mpya wa gesi katika Kitalu cha Mnazi Bay, kwenye kisima cha Kasa 1X, chenye makadirio ya futi za ujazo bilioni 223 za gesi asilia, Dkt. Homera amesema haiwezekani eneo linalozalisha kiasi kikubwa cha gesi nchini likakosa barabara ya kiwango cha lami.

Sauti ya Dkt Juma Homera Waziri wa Nishati

Nao baadhi ya wabunge kutoka majimbo mbalimbali ya Mkoa wa Mtwara wameeleza umuhimu wa rasilimali hiyo katika maendeleo ya taifa, huku wakiiomba Serikali kuweka kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu ya barabara Msimbati ili wananchi wanaozunguka na kulinda mradi huo wanufaike na uwepo wake.

Sauti ya baadhi ya wabunge mkoa wa Mtwara

Kwa upande wao, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara pamoja na Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Donald Wilson Msengi, wameitaka Serikali kuhakikisha ahadi zinazotolewa kwa wananchi zinatekelezwa kwa vitendo, hususan katika maeneo yanayozalisha rasilimali ya gesi asilia.

Sauti ya mwenyekiti wa CCM na Mkuu wa mkoa wa Mtwara

Wakieleza mahitaji yao ya msingi, wananchi wa Kata ya Msimbati wamesema wanatarajia kuona ahadi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ikitekelezwa, sambamba na kupatiwa huduma ya umeme bila malipo, ili nao waweze kunufaika na rasilimali ya gesi asilia inayozalishwa katika eneo lao.

Sauti ya baadhi ya wananchi wa Msimbati