Bodi ya pamba Bunda waelekezwa kuandaa kikao cha wadau kujadili changamoto
7 December 2024, 9:53 pm
Zao la pamba limepoteza kabisa ushawishi kwa wakulima kutokana na changamoto zake kwa sasa likiwemo suala la bei, pamoja na uzalishaji hafifu wa zao hilo.
Na Adelinus Banenwa
Kikao cha kama ya ushauri ya wilaya ya Bunda DCC kilichoketi tarehe 6 Dec 2024 kimeadhimia viongozi wa bodi ya pamba wilayani Bunda kuandaa kikao cha wadau wa zao la pamba ili kujadili changamoto za zao hilo.
Mwenyekiti wa kikao hicho Ndugu Salumu Mtelela ambaye ni katibu tawala wilaya ya Bunda kwa niaba ya Mhe mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt Vicent Naano pamoja na wajumbe wa kikao hicho wamefikia kutoa azimio hilo kutokana na kile kilichoelezwa changamoto nyingi zinazolikumba zao la pamba wilayani Bunda kwa sasa.
Katika michango yao wajumbe wa kikao hicho wamesema zao la pamba limepoteza kabisa ushawishi kwa wakulima kutokana na changamoto zake kwa sasa likiwemo suala la bei, pamoja na uzalishaji hafifu wa zao hilo.
Pia kamati hiyo imeazimia barabara ya Busambara – Mugara iliyopo halmashauri ya wilaya ya Bunda ambayo inaunganisha wilaya za Bunda na Musoma kuhamishwa kutoka TARURA na kuwa chini ya TANROADS ili itengenezwe kwa kiwango cha lami kutokana na umuhimu wake kiuchumi.
Kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya DCC kinalenga kupokea taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi kutoka halmashauri pamoja taasisi za serikali ambapo kwa Bunda kamati ilipokea taarifa za taasisi hizo ikiwemo TARURA, BUWSSA, RUWASA, TANESCO, Pamba, miongoni mwa taasisi zingine.
Akihairisha kikao hicho mwenyekiti wa kikao Ndugu Salumu Mtelela amesema maendeleo ya taaluma wilayani Bunda iko chini na hairidhishi hivyo ni jukumu la wadau wote wa elimu kuwa na mpango mkakati wa kuinua hali ya elimu wilayani Bunda.