Wanafunzi Chamtigiti kusomea chini ya mti, serikali yaweka mkono
11 August 2024, 9:47 am
Na Edward Lucas
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, George Stanley Mbilinyi, amesisitiza umuhimu wa kumalizia ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Chamtigiti, baada ya serikali kutenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya madarasa mawili kupitia miradi ya EP4R na BOOST ili kusaidia kilio cha wanafunzi kusomea chini ya mti na wengine kupokezana darasa.
Amesema madarasa mawili yanayojengwa kwa msaada wa wananchi tayari yameshapelekewa andiko TAMISEMI na yanahitaji kumaliziwa kwa jumla ya milioni 25.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 10 Agosti 2024, mbele ya Mbunge wa Jimbo la Bunda, Mheshimiwa Boniface Getere, Mwalimu Mkuu Emmanuel Godfrey Mahaga alieleza kuwa wanafunzi wa darasa la tatu wanalazimika kusoma chini ya mti kutokana na uchakavu wa darasa lao, na wanafunzi wa madarasa ya awali na la pili wanakumbana na upungufu wa madarasa.
Naye Mbunge wa jimbo la Bunda, Mhe. Boniface Mwita Getere amewasisitiza wananchi na viongozi wa eneo hilo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa maboma ya madarasa mawili kwa hatua za nguvu za wananchi ili serikali imalizie hatua zitakazokuwa zimesalia
Shule inahitaji madarasa 11, lakini ina madarasa 6 pekee, hali inayokwamisha shughuli za masomo.