Getere ataka ujenzi choo cha walimu Chamtigiti ukamilike
11 August 2024, 12:33 am
Na Edward Lucas
Mbunge wa jimbo la Bunda, Mhe. Boniface Mwita Getere amewaomba viongozi wa serikali ya kijiji na wadau wengine wa elimu kuhakikisha ifikapo tarehe 30 Septemba 2024 wawe wamekamilisha ujenzi wa choo cha walimu shule ya msingi Chamtigiti ili kuwaondolea walimu usumbufu wa kujisaidia vichakani au kurudi majumbani.
Getere ametoa ombi hilo leo 10 Aug 2024 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo hilo viwanja vya shule ya msingi Chamtigiti akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wakiongozwa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake jimboni kusikiliza kero za wananchi.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya shule, Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ndugu Emmanuel G. Mahaga sambamba na kubainisha mafanikio mbalimbali aliyopo alieleza pia changamoto zinazoikabiri shule hiyo kuwa ni pamoja na uchakavu wa choo cha wanafunzi na ukosefu wa choo cha walimu jambo ambalo huwafanya kwenda kujisaidia majumbani mwao hata wakati wa kazi
Shule ya msingi Chamtigiti iliyopo kata ya Hunyari ilisajiliwa mwaka 1990 kwasasa ina wanafunzi 485, ina walimu 7 wa serikali na wawili kutoka Grumeti hivyo kuwa na jumla ya walimu 9 kati yao wakiume ni 8 na mmoja ni wakike