Mkandarasi wa usafi atimuliwa Bunda kwa kushindwa kazi
17 February 2024, 10:06 pm
Halmashauri ya mji wa Bunda imetangaza kuvunja mkataba na mkandarasi wa usafi ndani ya mji wa Bunda kutokana na kushindwa kutekeleza mkataba wake.
Na Adelinus Banenwa
Halmashauri ya mji wa Bunda imetangaza kuvunja mkataba na mkandarasi wa usafi ndani ya mji wa Bunda kutokana na kushindwa kutekeleza mkataba wake.
Ufafanuzi huo umetolewa na Protas Majula afisa mazingira na usafi halmashauri ya mji wa Bunda katika mkutano wa hadhara wa ofisi ya mkurugenzi kusikiliza kero za wananchi kata ya Nyasura.
Majula amesema mkandarasi aliyekuwepo (MAGEREZA) alimaliza muda wake mwezi wa saba mwaka jana na hakuomba tena, huku kampuni iliyotuma maombi na kupata kandarasi hiyo imeonekana haina uwezo wa kuhudumia mji wa Bunda hivyo halmashauri imelazimika kuvunja mkataba na mkataba huo unakoma Feb 29, 2024 na tayari halmashauri imeshapata mkandarasi mwingine wa kufanya usafi mjini Bunda.
Diwani wa kata ya nayasura Magigi Samweli Kiboko amesema kile wanachokililia wananchi kuhusu mkandarasi wa usafi kweli ni changamoto na tayari kupitia baraza la madiwani walimuelekeza mkurugenzi kuchukua hatua kwa mkandarasi huyo kwa kuwa amekosa sifa na ameshindwa kazi,
Awali wananchi wa kata ya nyusura mbele ya Afisa utumishi aliyemuwakilisha Mkurugenzi walitoa malalamiko yao juu ya suala mkandarasi wa usafi kushindwa kazi jambo linalosababisha uchafu kuzagaa kila kona ndani ya mji wa Bunda.