Sekondari ya Nyiendo kuwekewa umeme vyumba sita vya madarasa
14 October 2023, 1:28 pm
Eng. Kambarage Wasira kwa kushirikiana na mdau wa maendeleo ndugu Eng.Gasper Mchanga wameahidi kuweka umeme katika madarasa 6 shule ya Sekondari Nyiendo iliyopo Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara.
Na Adelinus Banenwa
Mfumo wa umeme utakaogharimu shilingi milioni mbili laki moja na sabini na sita elfu (2,176,000) unatarajiwa kufugwa katika vyumba 6 vya madarasa shule ya Sekondari Nyiendo iliyopo kata ya Kabarimu halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara.
Akizungumza katika mahafali ya 16 ya wanafunzi wa kidato Cha nne Eng Kambarage Wasira mgeni rasmi katika mahafali hiyo amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto nyingi shuleni hapo lakini suala la kuwepo kwa nishati ya umeme katika madarasa kutawawezesha wanafunzi kujifunza kwa uhuru hasa wanaowahi kufika shuleni asubuhi na wale wanaochelewa kutoka hasa madarasa ya mitihani.
Kambarage amesema kwa kushirikiana na mdau wa maendeleo ndugu Eng.Gasper Mchanga wataweka umeme katika madarasa 6 ya shule hiyo ili iwe rahisi kwa wanafunzi kujisomea.
Aidha amewapongeza wazazi kwa kuhamasisha wanafunzi kwenda shule huku akiangazia idadi ya wanafunzi walioanza shule na wale walihitimu leo ikiwa ni tofauti ya wanafunzi watano tu.
Kupitia taarifa ya shule iliyosomwa na mkuu wa shule hiyo Merida Maeda mbele ya mgeni rasmi amesema changamoto kubwa shuleni hapo ni suala la umeme kwenye madarasa jambo linalosababisha wanafunzi wanaowahi shuleni asubuhi kushindwa kujisomea kutokana na kukosa mwanga pia changamoto ya ushirikiano kati ya wazazi na uongozi wa shule akibainisha wazazi kushindwa kuchangia chakula Cha watoto shuleni
Changamoto zingine ni matundu ya vyoo, matenk ya kuvunia maji ya mvua na maabala mbili pamoja na maktaba.
Awali wakisoma risala mbele ya mgeni Rasmi wanafunzi wa kidato Cha nne wamesema mwaka 2020 walianza shule wakiwa 185 kati yao wavulana 93 na wasichana 92 ambapo hadi wanahitimu wamebaki wanafunzi 180 na kufanya idadi ndogo ya wanafunzi ambao hawajamaliza shule.