Bunda: Wanafunzi watembea kilometa 16 hadi 20 kwa siku kufuata huduma ya elimu
21 April 2023, 7:20 am
Wakazi wa Kijiji Cha Nyaburundu katika Kata ya Ketare Halmashauri ya wilaya ya Bunda wameiomba serikali kuwakubalia kujenga shule ya secondary katika eneo walilolipendekeza kutokana na changamoto wanazokutana nazo watoto wao wanaokwenda kusoma shule ya Kijiji Jiran.
Wakizungumza katika kikao Cha hadhara wanakijiji hao wamesema walitenga eneo lililopo karibu na shule ya msingi Nyaburundu na tayari wameweka viashilia na ndilo eneo pekee lililopo katika Kijiji hicho.
Kupitia kwa wakazi hao wamesema changamoto za umbali takribani kilometa 8 hadi 10 kwenda tu shule ukiongeza kwenda na kurudi wanafunzi hutembea kilometa 16 hadi 20, pili changamoto ya wanafunzi wa kike kupata mimba ambapo kwa mwaka jana 2022 tu wanafunzi 16 wamepata mimba na ukiacha wale walioacha shule kwa sababu zingine.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji Cha Nyaburundu Hamis Said Madoro amesema anaiomba serikali kukubali kujengwa kwa shule katika eneo lililotengwa na Kijiji kwa kuwa tayari wameshapeleka viashilia pia eneo hilo lipo katikati ya Kijiji na ni rahisi kufikika kwa wanafunzi wote.
Radio Mazingira FM ilizungumza na wanafunzi wanaosoma shule ya secondari Esperanto kutokea Nyaburundu wamesema limekuwa ni jambo la mateso kwa kuwa huamka saa kumi Alfajil na kufika shuleni saa moja kasoro.
Wanafunzi hao wamebainisha kuwa wamekuwa katika kipindi kigumu mara nyingine hukimbizwa usiku na watu wasiyowajua wakati wakienda shule huku watoto wa kike wakihofia kubakwa.
Aidha wamesema kipindi Cha Mvua hali Huwa mbaya zaidi ambapo Mazingira FM iliwashuhudia wanafunzi hao wakiwa wamenyeshewa na mvua wengine wakiwa wameshikilia viatu huku wanatembea bila Peku.
Kupitia kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji Cha Nyaburundu akisoma maelekezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda amesema eneo lililopendekezwa na Kijiji halitoshi kujenga shule ya secondari na eneo hilo ni Mali ya shule ya msingi Nyaburundu hivyo wanakijiji hawapaswi kulitumia badala yake watafute eneo lingine.