FM Manyara
FM Manyara
10 November 2026, 4:38 pm

Benki ya CRDB imekabidhi darasa moja pamoja na madawati 50 vyenye thamani ya shilingi milioni 25 kwa Shule ya Sekondari Magugu iliyopo Wilaya ya Babati mkoani Manyara, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuunga mkono sekta ya elimu nchini.
Na Mzidalfa Zaid
Serikali wilayani Babati mkoani Manyara imeishukuru Benki ya CRDB kwa kujenga darasa pamoja na madawati katika Shule ya sekondari Magugu, ambapo darasa hilo litasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo ,Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB Adimin Mwansasu, amesema benki hiyo kila mwaka hutenga asilimia moja ya faida yake kwa ajili ya kurejesha sehemu ya mapato hayo kwa jamii kupitia kusaidia sekta za afya, elimu na mazingira, ambapo Shule ya Sekondari Magugu imekuwa miongoni mwa wanufaika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Hashim Mgandilwa, ameishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huo akisema utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa na madawati, huku ukiwawezesha wanafunzi kujifunza katika mazingira bora.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Magugu Revocatus Kimario amesema awali shule hiyo ilikuwa na upungufu wa madarasa matano, lakini kufuatia msaada huo, changamoto hiyo imepungua na kubaki na upungufu wa madarasa manne.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wameishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huo wakieleza kuwa awali walikabiliwa na changamoto ya upungufu wa madawati, hali iliyokuwa ikiathiri mazingira yao ya kujifunzia, huku wakiamini msaada huo utawasaidia kujifunza na kujisomea vizuri.
