FM Manyara
FM Manyara
14 June 2026, 2:54 pm

Shule ya Deira English Medium imeendelea kuthibitisha ubora wake wa kitaaluma kwa kuandaa hafla maalum ya kuwapongeza na kuwazawadia wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao, hatua inayodhihirisha dhamira ya shule hiyo ya kuendeleza ufaulu na kukuza vipaji vya wanafunzi.
Na Mzidalfa Zaid
Hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya shule hiyo iliwakutanisha wanafunzi, wazazi, walimu na viongozi mbalimbali wa shule kwa lengo la kutambua mafanikio ya wanafunzi waliomaliza Darasa la Saba mwaka 2021 na kupata matokeo ya Single Digit katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, pamoja na wanafunzi waliomaliza Darasa la Nne mwaka jana na ambao kwa sasa wapo Darasa la Tano.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Shule ya Deira English Medium, Nada Shauri Nada, alisema kuwa utoaji wa zawadi hizo ni sehemu ya kutimiza ahadi aliyowahi kuitoa kwa wanafunzi wakati wa mahafali ya mwaka 2021, lakini pia ni njia ya kuwapa motisha wanafunzi wengine kujituma zaidi katika masomo yao.

Kwa upande wao wanafunzi waliomaliza Kidato cha Nne na kupata matokeo ya Single Digit, walikabidhiwa zawadi mbalimbali ikiwemo shilingi laki Tano kwa Kila Mmoja ikiwa ni ishara ya kuthamini juhudi zao zilizowafanya kuendelea kufanya vizuri tangu walipokuwa katika shule hiyo ya msingi huku wakielezea furaha yao kwa kutambuliwa na kupewa zawadi, wakisema hatua hiyo imewaongezea hamasa ya kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao na kufikia malengo makubwa zaidi ya kielimu.

Katika hafla hiyo pia wanafunzi waliomaliza Darasa la Nne mwaka jana na ambao kwa sasa wanasoma Darasa la Tano katika shule hiyo walipongezwa kwa kufanya vizuri kitaaluma na kukabidhiwa zawadi mbalimbali mbele ya wazazi wao ambapo Wanafunzi hao walieleza kufurahishwa na hatua ya shule kuwathamini tangu wakiwa katika madarasa ya chini.

Baadhi ya wazazi waliohudhuria hafla hiyo waliishukuru menejimenti ya shule kwa kuendelea kuthamini juhudi za wanafunzi na kuwekeza katika kukuza taaluma.
Mkuu wa Shule hiyo, Bosco Godfrey, amesema hafla hiyo imekuwa sehemu ya utamaduni wa shule wa kuthamini mafanikio ya wanafunzi na kuimarisha ushirikiano kati ya shule, wanafunzi na wazazi.
Kwa upande wake Makamu Mkurugenzi wa shule hiyo, Ursula John, amesema shule itaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuinua kiwango cha taaluma na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora yatakayowawezesha kufikia ndoto zao.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shule, Kibiki Kibiki, aliipongeza menejimenti ya shule kwa kuendelea kuwekeza katika elimu bora na kuwahamasisha wanafunzi kufanya vizuri.
Aidha, walimu nao wamepata zawadi ya shilingi milioni moja wa madarasa ya mtihani ambao wamepelekea wanafunzi kufaulu vizuri ambapo wametoa shukrani kwa uongozi wa shule hiyo huku uongozi wa shule ukitoa zaidi ya shilingi milloni saba kwa ajili ya walimu wote wa shule hiyo.
