FM Manyara

TAKUKURU yabaini ubadhirifu mradi wa shule Simanjiro

25 May 2026, 6:05 pm

Picha ya Naibu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Manyara Anthony Gang’olo

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Manyara imefanikiwa kudhibiti upotevu wa zaidi ya Shilingi milioni mbili katika mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Namalulu iliyopo wilayani Simanjiro baada ya kubaini matumizi mabaya ya fedha za mradi huo.

Na Mzidalfa Zaid

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Manyara Anthony Gang’olo amesema  kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2026 walibaini kuwepo kwa ubadhirifu katika matumizi ya fedha za ujenzi wa madarasa matatu na vyoo vya matundu sita katika shule hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Mtendaji wa Kijiji cha Namalulu ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa mradi alinunua mchanga wa lori mbili kwa Shilingi 1,200,000 huku thamani halisi ya soko ikiwa Shilingi 450,000 jambo lililosababisha hasara ya Shilingi 750,000 kwa Serikali.

Amesema ilibainika kuwa kokoto za lori mbili zilinunuliwa kwa Shilingi 2,000,000 wakati bei halisi ya soko ilikuwa Shilingi 1,225,000 na kusababisha hasara nyingine ya Shilingi 775,000.

Sauti ya Naibu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Manyara Anthony Gang’olo

Katika hatua nyingine, TAKUKURU ilibaini kuwepo kwa makisio yasiyo halisi ya mbao za ujenzi ambapo mbao 45 ziliripotiwa kupokelewa zaidi ya kiwango halisi na kuisababishia Serikali hasara ya Shilingi 525,000.

Kutokana na uchunguzi huo, TAKUKURU imefanikiwa kurejesha fedha zote zilizopotea zenye thamani ya Shilingi 2,050,000.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama Cha waandishi wa habari mkoa wa Manyara Zacharia Mtigandi , ameipongeza TAKUKURU kwa kuwaita waandishi wa habari mkoa wa Manyara na kutoa elimu  inayohusu TAKUKURU ambapo amesema hatua hiyo inaleta ushirikiano baina ya Taasisi hiyo na waandishi wa habari.

Sauti ya mwenyekiti wa chama Cha waandishi wa habari mkoa wa Manyara Zacharia Mtigandi
Picha ya mwenyekiti wa chama Cha waandishi wa habari mkoa wa Manyara Zacharia Mtigandi