FM Manyara
FM Manyara
19 August 2026, 2:30 pm

Kampeni ya chanjo ya polio kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka kumi inatarajiwa kuanza Agosti 27 hadi 30, 2026, katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Na Mzidalfa Zaid
Akizungumza na FM Manyara, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, James Mleli, amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza ulinzi kwa watoto dhidi ya ugonjwa wa polio, ambao unaweza kusababisha ulemavu wa kudumu.
Mleli amesema chanjo hiyo itatolewa bila malipo katika vituo vya kutolea huduma za afya, nyumba kwa nyumba, shule, pamoja na maeneo mengine yatakayotengwa kwa ajili ya zoezi hilo.
Ameongeza kuwa kampeni hiyo itawahusu watoto wote wenye umri wa chini ya miaka kumi, wakiwemo wale ambao tayari wamewahi kupata chanjo ya polio, huku akiwataka wazazi na walezi kushirikiana na wahudumu wa afya ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.
Mleli amewataka wananchi kuchangamkia kampeni hiyo na kuwapeleka watoto kupata chanjo kwa kuwa kinga dhidi ya polio ni muhimu katika kulinda afya na maisha ya watoto.