FM Manyara
FM Manyara
21 September 2026, 2:08 pm

Kambi ya matibabu iliyoratibiwa na Shirika la So They Can Tanzania (STC) imekamilika rasmi wilayani Babati
Na Marino Kawishe
Zaidi ya wananchi 1,800 wamepata huduma mbalimbali za afya, ikiwemo uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake, uchunguzi wa macho, vipimo vya kinywa na meno, pamoja na uchunguzi wa afya ya akili na ushauri nasaha.
Akizungumza kuhusu huduma zilizotolewa katika kambi hiyo, Muuguzi Mkuu kutoka Hospitali ya Wilaya ya Babati, Sister Thea Funto, amesema kambi hiyo imekamilika huku akilishukuru Shirika la So They Can Tanzania pamoja na watoa huduma wote walioshiriki kutoa huduma kwa siku sita katika maeneo yaliyofikiwa na kambi hiyo.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wananchi waliojitokeza katika kambi hiyo wamebainika kuwa na changamoto za uoni hafifu pamoja na usikivu duni, hali inayosisitiza umuhimu wa wananchi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini changamoto mbalimbali za kiafya mapema.
Akibainisha hilo, Mratibu wa Idara ya Macho kutoka Hospitali ya Wilaya ya Babati, Dkt. Silvia Nyange, amesema baadhi ya wananchi hawafanyi uchunguzi wa afya kwa wakati, jambo ambalo linaweza kuchelewesha kubainika kwa changamoto mbalimbali za kiafya.
Naye Mtaalamu wa Uchunguzi wa Masikio na Macho kwa Watoto kutoka Chuo cha Elimu Maalumu Patandi, Xavery Haule, amesema katika kambi hiyo wameweza kuwafanyia uchunguzi wananchi pamoja na watoto na kubaini baadhi yao wakiwa na matatizo ya masikio ambayo yanaweza kuathiri uwezo wao wa kusikia.
Amesema baadhi ya watoto walikutwa na vitu kama wadudu na vitu vingine masikioni, hali ambayo inaweza kusababisha usikivu hafifu endapo haitapatiwa matibabu kwa wakati.

Kambi hiyo ya matibabu imekamilika Septemba 19 mwaka huu, ikiwa imefanikiwa kuwafikia wananchi na kutoa huduma mbalimbali kwa kushirikisha wataalamu kutoka Hospitali ya Wilaya ya Babati pamoja na wadau wengine wa afya.
Kumalizika kwa kambi hiyo pia kumekuwa sehemu ya maandalizi ya kuendelea na huduma kama hizo katika kipindi kijacho, ambapo maandalizi ya kambi nyingine yanatarajiwa kufanyika mwakani, 2027.
