FM Manyara
FM Manyara
15 November 2026, 3:04 pm

Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Babati mkoani Manyara kimefanya operesheni maalum ya ukaguzi wa magari yanayounganisha wilaya tatu za Babati, Hanang’ na Mbulu, kwa lengo la kuhakikisha madereva wanazingatia sheria na kanuni za usalama barabarani katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka.
Na Emmy Peter
Akiongoza operesheni hiyo, DTO wa Wilaya ya Babati, Emmanuel Kandola, amesema ukaguzi huo unalenga kuhakikisha magari yanayotumika kusafirisha abiria yanakidhi vigezo vya usalama, kuwabaini madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani pamoja na wale wanaotumia vilevi wanapokuwa safarini.
Kwa upande wao, DTO wa Wilaya ya Hanang’, Ambwene Mwasubila, na DTO wa Wilaya ya Mbulu, Hassan Karatha, wamesema operesheni hiyo ni sehemu ya ushirikiano baina ya wilaya hizo katika kuzuia ajali za barabarani, kudhibiti magari mabovu yanayoendelea kutoa huduma za usafirishaji na kuhakikisha madereva wanazingatia sheria za usalama barabarani wakati wote wa safari.
operesheni hiyo inalenga kulinda usalama wa abiria na mali zao ili kuhakikisha wanafika katika maeneo yao ya safari salama, pamoja na kupunguza ajali zinazoweza kusababishwa na uzembe wa madereva, hususan katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.