FM Manyara

Zaidi ya walimu laki tatu kunufaika na mafunzo ya sayansi na teknolojia kupitia MEWAKA

16 October 2026, 9:48 pm

Picha ya walimu, wanafunzi pamoja na mwakilishi wa Vodacom Tanzania

Zaidi ya walimu laki tatu nchini wanatarajiwa kunufaika na mpango wa kupata mafunzo na nyenzo za kufundishia kupitia mfumo wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA), katika eneo la sayansi na teknolojia, hatua inayolenga kuimarisha maarifa na ujuzi wa walimu kwa ajili ya kuboresha utoaji wa elimu bora nchini.

Na Mzidalfa Zaid

Kupitia mfumo wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA), walimu zaidi ya laki tatu nchini wanatarajiwa kupata fursa ya kujiendeleza kitaaluma katika sayansi na teknolojia,

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo cha kwanza cha rasilimali kwa walimu kati ya vituo 50 vinavyotarajiwa kujengwa na Vodacom Tanzania Foundation nchini, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Zuweina Faraa, amesema wamejipanga kuwezesha vituo hivyo kwa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na huduma ya intaneti ili kuwawezesha walimu kupata mafunzo na nyenzo mbalimbali za kufundishia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, baada ya kuzindua kituo hicho kilichopo katika Shule ya Msingi Naurei, ameitaka jamii ya eneo hilo kukilinda na kukitunza ili kiendelee kutoa huduma zilizokusudiwa, akisema uwepo wa kituo hicho ni fursa muhimu kwa walimu na jamii kwa ujumla.

Naye mwalimu wa Shule ya Msingi Naurei, Marry Mpanduji, ambaye ni miongoni mwa walimu watakaonufaika na kituo hicho, amesema kitawasaidia kuongeza ujuzi na kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani, hususan katika ufundishaji na ujifunzaji.

Agnes Laizar ni mkazi wa Kijiji cha Naurei, ameonesha furaha yake kutokana na kuanzishwa kwa kituo hicho, akieleza matumaini yake kuwa kitakuwa na manufaa kwa walimu na jamii inayozunguka eneo hilo.