FM Manyara
FM Manyara
5 October 2026, 11:01 pm

Mkuu mpya wa Wilaya ya Babati Hashim Shaibu, amekabidhiwa rasmi ofisi ya mkuu wa wilaya ya Babati na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Emanuela Kaganda katika hafla fupi iliyofanyika leo katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Babati.
Na Mzidalfa Zaid
Mkuu wa wilaya ya Babati Hashim Shaibu ameahidi kushughulikia migogoro ya ardhi pamoja na pombe haramu katika wilaya ya Babati.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Hashim Shaibu, ameahidi kushughulikia changamoto ya migogoro ya ardhi pamoja na matumizi ya pombe haramu katika Wilaya ya Babati.
Shaibu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo ya kulitumikia Taifa, akisema atahakikisha anaendeleza kazi na majukumu yaliyoachwa na mtangulizi wake.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Wilaya ya Babati, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emanuela Kaganda, amewashukuru wananchi wa Babati kwa ushirikiano waliompa wakati wa uongozi wake, akisema ushirikiano huo ulimsaidia kutekeleza majukumu yake na kushughulikia changamoto mbalimbali za wananchi.
Naye aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Babati, Remidius Mwema, amemtakia kila la heri Mkuu huyo mpya katika majukumu yake mapya, huku akimuomba kuendeleza kazi alizoachiwa na watangulizi wake.
