FM Manyara

Elimu ya uraia na utawala bora kuleta mabadiliko Mbulu

29 October 2026, 8:42 pm

Picha ya baadhi ya watendaji wa wilaya ya mbulu

Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara wamejipanga kutumia elimu ya Uraia na Utawala Bora waliyoipata kupitia mafunzo yanayotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ushirikishwaji wa wananchi na kuboresha utoaji wa huduma katika maeneo yao ya kazi.

Na Mzidalfa Zaid

watumishi hao wamesema maarifa waliyoyapata yatawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, ikiwemo uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika halmashauri hiyo, Zabron Kabazi, amesema uelewa wa masuala ya Uraia na Utawala Bora ni msingi wa kujenga jamii yenye amani na mshikamano, sambamba na kuweka mazingira yanayochochea shughuli za kiuchumi na maendeleo endelevu.

Amesema elimu hiyo ni muhimu kwa watumishi wa umma kwa kuwa inawasaidia kutambua wajibu wao katika kutekeleza majukumu ya Serikali na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Picha ya mgeni rasmi pamoja na watumishi kutoka ofisi ya wizara ya katiba na Sheria

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kijiji katika halmashauri hiyo, Mariam Mtani, amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika utendaji wa watumishi, akiwataka watumishi wenzake kutumia maarifa waliyoyapata kuboresha utendaji wao na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji, Zuhura Salehe, amesema atatumia elimu hiyo kuwafikia wananchi wa kijiji chake ili kuongeza uelewa wao kuhusu uraia na utawala bora na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Amesisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ni muhimu katika kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha miradi hiyo inakidhi mahitaji ya jamii.

Ameongeza kuwa utoaji wa elimu ya uraia utawasaidia wananchi kuelewa haki na wajibu wao na hivyo kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo katika maeneo yao.

Awali, akifungua mafunzo hayo Oktoba 29, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Mbwana Rajabu Kambangwa, amesema elimu ya Uraia na Utawala Bora ni nyenzo muhimu katika kujenga uwezo wa viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa.

Picha ya baadhi ya washiriki