FM Manyara
FM Manyara
4 September 2026, 6:14 pm

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martine Shigela, amekabidhiwa rasmi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, ambaye awali alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Na Mzidalfa Zaid
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi hiyo, RC Shigella amewaomba wananchi wa Mkoa wa Manyara kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake, huku akiahidi kuendeleza shughuli za maendeleo zilizoanzishwa na uongozi uliopita.
Katika hatua nyingine, RC Shigella amewataka wananchi wa Mkoa wa Manyara kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi katika maeneo yote ya mkoa ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, amesema Mkoa wa Manyara umeendelea kukua kiuchumi, huku akiahidi kumpa ushirikiano RC Shigella kwa kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu mkoa huo pale utakapohitajika.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Mkoa wa Manyara, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Remidius Mwema, amesema viongozi wa mkoa huo walifanya kazi kwa ushirikiano na RC Queen Sendiga wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, na kwamba wataendeleza ushirikiano huo na Mkuu wa Mkoa mpya, Martine Shigella.
