FM Manyara

Zaidi ya wananchi 1800 wanufaika na kambi ya madaktari bingwa Manyara

24 April 2026, 6:46 pm

picha ya kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Manyara Dokta Yesige Mutajwaa

Zaidi ya wananchi 1800 wamenufaika kwa kufanyiwa uchunguzi na matibabu katika kambi maalum ya matibabu na upasuaji katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Manyara na kuhudumiwa na madaktari bingwa na wataalamu bobezi kutoka Marekani kuanzia april 19 hadi april 24,2026.

Na Mzidalfa Zaid

Hayo yameelezwa leo na  kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Manyara Dokta Yesige Mutajwaa wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake, amesema katika kipindi hicho cha april 19 hadi april 24  kumetolewa  matibabu ya upasuaji maalum( plastic surgery ) kurekebisha makovu yaliyotokana na ajali au moto, matibabu ya mdomo sungura,upasuaji wa jumla, huduma za pua, sikio, koo, macho ,matibabu ya mifupa, matibabu ya magonjwa ya wanawake na uzazi pamoja na uchunguzi wa saratani.

sauti ya kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Manyara Dokta Yesige Mutajwaa

Mutajwaa amesema katika kipindi hicho jumla ya wagonjwa 77 wamefanyiwa oparesheni katika maeneo mbalimbali ambapo amewashukuru wadau wote ambao wamepelekea kuendesha kambi hiyo.

Aidha, amewasisitiza wananchi kuendelea kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya wanapohisi dalili za kuumwa ili wafanyiwe matibabu pamoja na ushauri kabla magonjwa hayajawa sugu.