FM Manyara
FM Manyara
4 July 2026, 6:45 pm

Na Emmy Peter
Wananchi wa Kijiji Cha Endanoga Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara wamepatiwa mafunzo ya kilimo bora cha maharage kupitia mradi wa kuendeleza kilimo na uvuvi unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Selian.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea wakulima uelewa kuhusu matumizi ya mbegu bora za maharage zilizofanyiwa utafiti na TARI, pamoja na mbinu za kisasa za uzalishaji ili kuongeza mavuno na kuinua kipato cha kaya kupitia kilimo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mtafiti Mkuu kutoka TARI Selian, Frank Mmbando, amesema matumizi ya mbegu bora pamoja na kuzingatia kanuni sahihi za kilimo ni hatua muhimu katika kuongeza tija, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha maisha ya wakulima ambapo Mahagare hayo ni sehemu ya kuboresha lishe.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Pascal Mahetu, aliwataka wakulima kuyatumia kwa vitendo mafunzo waliyopata ili kuongeza uzalishaji wa maharage na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo katika eneo hilo.
Kwa upande wao wakulima walioshiriki mafunzo hayo wameshukuru TARI Selian kwa kuwafikia na kuwapatia elimu ya kilimo cha kisasa, wakieleza kuwa maarifa waliyoyapata yatawasaidia kuboresha uzalishaji na kuongeza mavuno katika misimu ijayo ya kilimo Cha Maharage.