FM Manyara
FM Manyara
22 May 2026, 7:26 pm

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini imefanya ziara ya kukagua na kutoa elimu ya maadili katika shule mbalimbali wilayani Babati ikiwa ni sehemu ya awamu ya pili ya utekelezaji wa programu ya vilabu vya maadili mashuleni.
Na Mzidalfa Zaid
Katika ziara hiyo, jumla ya shule 15 zimefikiwa ambapo shule 5 zipo Halmashauri ya Wilaya ya Babati na shule 10 zipo Halmashauri ya Mji wa Babati, lengo likiwa ni kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu maadili, uzalendo na uwajibikaji katika jamii.
Hayo yamesemwa na Afisa Maadili kutoka Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini, Adam Kuhanda, amesema kupitia ziara hiyo wanafunzi wameendelea kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili mema, nidhamu pamoja na kujiepusha na vitendo visivyofaa vinavyoweza kuharibu maisha yao na mustakabali wa taifa.

Kwa upande wao, wanafunzi kutoka shule mbalimbali zilizotembelewa wameeleza kuwa elimu hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwao kwani imewasaidia kuongeza nidhamu, kuwajibika katika masomo pamoja na kutambua umuhimu wa kuheshimu sheria na maadili ya jamii.

Nao baadhi ya walimu wakuu pamoja na walezi wa vilabu vya maadili kutoka shule mbalimbali wameipongeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuendelea kutoa elimu hiyo mashuleni wakisema imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha tabia na mwenendo wa wanafunzi.
Walimu hao wamesema uwepo wa vilabu vya maadili umeongeza mwamko wa wanafunzi kushiriki katika shughuli za maendeleo na kujenga mazingira bora ya kujifunza huku wakiiomba serikali kuendelea kuviimarisha vilabu hivyo ili viweze kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.

