FM Manyara
FM Manyara
9 August 2026, 1:59 pm

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga amewataka wananchi wa Mkoa wa Manyara na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki katika Mbio za Tanzanite Manyara Marathon zinazotarajiwa kufanyika Agosti 22, 2026, wilayani Babati, huku akieleza kuwa ushiriki wao utasaidia kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa watoto njiti.
Na Mzidalfa Zaid
Mhe. Sendiga ametoa wito huo leo baada ya kushiriki mazoezi ya pamoja na wananchi mkoani Manyara, ambayo ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha na kujiandaa kushiriki katika mbio hizo.
Hadi sasa zaidi ya washiriki 1,500 wamekwishajiandikisha, huku lengo likiwa ni kufikisha washiriki 3,000 kabla ya siku ya mashindano ambapo Mbio hizo zitahusisha 200m kwa watoto, kilomita 5, 10, 21 na 42, huku washindi katika makundi mbalimbali wakitarijiwa kupata zawadi ikiwemo fedha taslimu na tuzo.
Mhe. Sendiga amesema ushiriki wa wananchi katika mbio hizo ni zaidi ya kushiriki michezo, bali ni sehemu ya kuchangia jitihada za kuokoa maisha ya watoto wanaohitaji huduma maalumu za afya.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Suten Mwabulambo, amesema mbio hizi zitasaidia kuokoa maisha ya watoto wachanga na watoto njiti.
Aidha, baadhi ya viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya na wabunge wamesema wamejipanga kushiriki katika mbio hizo huku wakielezea namna watakavyohamasisha wananchi kushiriki katika mbio hizo za hisani.
Tanzanite Manyara Marathon inalenga kuchangisha zaidi ya shilingi bilioni 1.5, ambazo zitatumika kuboresha huduma za afya kwa watoto njiti, ikiwemo ujenzi wa jengo la huduma za watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang pamoja na ununuzi wa vifaa tiba katika Vituo vya huduma vya Afya katika Mkoa wa Manyara.