FM Manyara
FM Manyara
18 August 2026, 4:10 pm

Wananchi mkoani Manyara wametakiwa kutambua wajibu na mipaka yao katika jamii ili kusaidia kupunguza vitendo vya ukatili, hususan ukatili dhidi ya watoto na ukatili wa kijinsia.
Na Mzidalfa Zaid
Wito huo umetolewa leo na Afisa wa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto Mkoa wa Manyara, Leokadia Manya, wakati akizungumza na FM Manyara, ambapo amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili.
Leokadia amesema wazazi wanapaswa kuwa makini katika kuwapatia watoto simu za mkononi, akieleza kuwa matumizi yasiyodhibitiwa ya simu yanaweza kuwaweka watoto katika mazingira hatarishi na kuwafanya kukutana na maudhui au vitendo vinavyoweza kuchochea ukatili.
Kwa upande wake, Afisa wa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto Mkoa wa Manyara, Maige Kulwa, amesema madhara ya mtu kufanyiwa ukatili yanaweza kuwa makubwa, ikiwemo kupata ulemavu, kuathirika kwa afya ya akili, kupata magonjwa mbalimbali na hata kupoteza maisha.
Aidha, Maige amesema kuna sheria zinazomlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo amewataka wananchi kuzifahamu na kutoa taarifa pale wanapobaini mtoto yuko katika mazingira ya ukatili au hatarini kufanyiwa ukatili.
