FM Manyara

Wanahabari Manyara wajengewa uwezo kampeini ya chanjo ya matone ya polio

20 August 2026, 8:01 pm

Picha ya baadhi ya wanahabari wakipatiwa elimu kuhusu kampeini ya chanjo ya matone ya polio

Wanahabari mkoani Manyara wamejengewa uelewa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo ya Polio, hasa kuelekea kampeni ya utoaji wa chanjo ya matone ya Polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 10 ambapo wametakiwa kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo.

Na Mzidalfa Zaid

Hayo yamesemwa Mkoani Manyara na Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Maryam Muhaji, wakati akifungua mafunzo kuhusu Kampeni ya chanjo ya matone ya Polio kwa wanahabari, Maafisa Habari wa Mkoa na Halmashauri pamoja na watengeneza maudhui mitandaoni.

Mafunzo hayo yameandaliwa kuelekea Kampeni ya Chanjo ya Polio ya Matone, inayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026, kwa lengo la kuwafikia watoto walio chini ya umri wa miaka 10.

Muhaji amesema chanjo ya Polio ni muhimu katika kumkinga mtoto dhidi ya ugonjwa huo, hivyo wanahabari wana nafasi kubwa ya kutumia majukwaa yao kutoa elimu sahihi na kuhamasisha wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata chanjo.

Sauti ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Maryam Muhaji
Picha ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Maryam Muhaji

Kwa upande wake, Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, Wizara ya Afya, Dr. Mwendwa Mwenesi amesema ugonjwa wa Polio unaweza kuambukizwa kwa kutozingatia kanuni za usafi, ikiwemo kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa virusi hivyo, amesisitiza umuhimu wa jamii kuzingatia usafi wa mazingira na usafi binafsi.

Sauti ya Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, Wizara ya Afya, Dr. Mwendwa Mwenesi

Naye Simon Nzilibili kutoka Wizara ya Afya amewataka wanahabari kutumia taaluma yao kuandika habari zinazolenga kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya, akisisitiza kuwa taarifa sahihi zina mchango mkubwa katika kujenga uelewa na kuondoa dhana potofu.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Andrew Method, amewataka wanahabari kuzingatia weledi katika utoaji wa taarifa kuhusu masuala ya afya na kuepuka habari zinazoweza kuzua taharuki au mkanganyiko kwa wananchi.

Afisa afya wa mkoa wa Manyara, Suten Mwabulambo, amesema kampeni hiyo itahusisha maeneo mbalimbali ili kuhakikisha watoto wote walio katika kundi lengwa wanafikiwa na kupata chanjo hiyo.

Sauti ya afisa afya wa mkoa wa Manyara, Suten Mwabulambo,

Baadhi ya wanahabari walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kupata elimu kuhusu chanjo ya Polio, wakiahidi kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo na kutoa taarifa sahihi kwa wananchi.

Sauti ya Baadhi ya wanahabari

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, jumla ya watoto 6,555,511 wanatarajiwa kufikiwa na chanjo katika mikoa nane inayoshiriki kampeni hiyo ambapo Mikoa hiyo ni Manyara, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Mara na Mkoani Manyara, jumla ya watoto 675,630 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya matone ya Polio katika kampeni hiyo.