FM Manyara
FM Manyara
23 September 2026, 6:55 am

Serikali mkoani Manyara imekutana na Mashirika yasiyo ya kiserikali kujadili masuala muhimu yanayofanywa na Mashirika hayo.
Na Mzidalfa Zaid
Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Manyara yametakiwa kuzingatia na kuheshimu mila, desturi na utamaduni wa kitanzania wakati wa kutekeleza shughuli zao, ili kuhakikisha miradi na programu wanazozitekeleza zinaendana na mazingira ya jamii wanazozihudumia.
Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Manyara, Dora Mziray, alipokuwa mgeni rasmi katika Jukwaa la Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali Mkoa wa Manyara, ambapo amesisitiza umuhimu wa mashirika hayo kufanya kazi kwa kushirikiana na jamii, pamoja na kuzingatia taratibu na maadili yanayotambulika katika jamii za kitanzania.

Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali Mkoa wa Manyara, Anna Fisso, ameyataka mashirika kuweka wazi taarifa muhimu zinazohusu shughuli zao, ikiwemo aina ya shughuli wanazotekeleza, maeneo wanayofanyia kazi na namna wanavyowahudumia wananchi, ili kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa NACONGO, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Impact Lead Tanzania Yohana Justine amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo katika sekta za kijamii, afya, elimu na maeneo mengine yenye manufaa kwa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
