FM Manyara
FM Manyara
8 November 2026, 11:17 am

Mwenyekiti wa Makampuni ya Mati Groups, David Mulokozi, amechangia Shilingi milioni 100 kupitia yeye, familia yake na kampuni hiyo katika harambee ya kuchangia miradi ya maendeleo ya Jimbo Katoliki la Mbulu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa jimbo hilo.
Na Mzidalfa Zaid
kuelekea Maadhimisho ya Jubilei ya Almasi ya miaka 75 ya Jimbo Katoliki la Mbulu yanatarajiwa kufanyika Machi 2028, Mwenyekiti wa Makampuni ya Mati Groups, David Mulokozi amechangia shilingi million 100 kusaidia miradi ya kanisa.
Akizungumza katika harambee hiyo iliyofanyika ndani ya Dekania ya Babati, Mulokozi amesema mchango huo unatokana na imani yake kwa Mungu, akieleza kuwa kila alichonacho ni zawadi kutoka kwa Mungu na hivyo kujitolea kwa ajili ya nyumba za ibada ni sehemu ya ibada na si suala la kujionyesha.
Amesema anaamini kila anachokifanya katika kusaidia maendeleo ya Kanisa ni kama kujiwekea nadhiri mbele za Mungu, huku akihimiza jamii kujenga utamaduni wa kujitolea na kuchangia maendeleo ya nyumba za ibada kulingana na uwezo wao.
Akisoma taarifa ya harambee hiyo, Dekano wa Dekania ya Babati, Reginald Kimati, amesema jumla ya fedha zilizopatikana pamoja na ahadi zilizotolewa zimezidi Shilingi milioni 200, huku lengo la jumla la jimbo likiwa kukusanya Shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa hosteli za malazi, ukumbi, jukwaa la kudumu la maadhimisho ya kijimbo pamoja na sehemu ya ujenzi wa kituo cha kichungaji Babati.
Akiongoza ibada hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu, Mhashamu Anthony Lagwen, amempongeza Mulokozi kwa moyo wake wa kujitolea na unyenyekevu, huku akisisitiza kuwa fedha zitakazopatikana zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

Maadhimisho ya Jubilei ya Almasi ya miaka 75 ya Jimbo Katoliki la Mbulu yanatarajiwa kufanyika Machi 2028, ikiwa ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa jimbo hilo Machi 25, 1953.
