FM Manyara
FM Manyara
7 October 2026, 11:04 pm

Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Manyara imepokea maafisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), waliotoa mafunzo kwa watumishi wa Idara hiyo kuhusu umuhimu wa kuzuia, kupambana na kujiepusha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Na Mzidalfa Zaid
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ya Uhamiaji mkoa wa Manyara, yamelenga kuwajengea watumishi uelewa kuhusu madhara ya rushwa, namna ya kutambua mazingira yanayoweza kuchochea vitendo hivyo, pamoja na umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa kutoka TAKUKURU, Paschal Justine Mhagama, amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kuzingatia maadili, uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao, huku akiwataka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Aidha, watumishi hao wamehimizwa kutambua na kuepuka matamshi, mienendo na vitendo vinavyoweza kusababisha upendeleo, rushwa au ukiukwaji wa taratibu, hali inayoweza kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake naibu afisa uhamiaji mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi Beatrice Alfred Bwire, ameishukuru TAKUKURU kwa kutoa mafunzo hayo, akisema yamekuwa muhimu katika kuongeza uelewa na kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, huku akiwataka watumishi kuendelea kuzingatia misingi ya uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
