FM Manyara
FM Manyara
17 September 2026, 9:15 pm

Wananchi wilayani Babati mkoani Manyara wametakiwa kuchangamkia fursa ya matibabu bure
Na Marino Kawishe
Zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya kumalizika kwa kambi ya afya inayotoa huduma za matibabu katika baadhi ya kata wilayani Babati, mkoani Manyara, wananchi wametakiwa kuchangamkia fursa hiyo ya matibabu bure kabla ya kambi hiyo kufungwa Jumamosi, Septemba 19, mwaka huu.
Akitoa tathmini ya ziara yake katika kambi hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo, amelishukuru shirika la So They Can Tanzania pamoja na wadau wote walioshirikiana na madaktari kutoka Hospitali ya Wilaya ya Babati katika kutoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi.

Aidha, Mbogo amewataka wananchi wa kata zilizobaki ambazo ni Endakiso na Mamire kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo za afya ambazo zinatolewa bure, huku akiwataka kuachana na dhana ya kusubiri siku ya mwisho ya kambi, hali ambayo inaweza kuwafanya baadhi yao kukosa huduma.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi huyo ametembelea kambi ya afya iliyopo Kata ya Qash, ambapo pia alipata fursa ya kupata huduma za uchunguzi wa macho na masikio.