FM Manyara
FM Manyara
21 June 2026, 7:19 am

Kuelekea maadhimisho ya siku ya wajane Duniani yanayoadhimishwa Juni 23 kila mwaka, Halmashauri ya Mji wa Babati imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko, mikutano ya kijamii na vyombo vya habari kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu haki za wajane na nafasi yao katika maendeleo ya jamii.
Na Mzidalfa Zaid
Hayo yameelezwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Mwanaidi Mwacha, ambaye amesema elimu hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutambua, kuheshimu na kulinda haki za wajane pamoja na kuwapa ushirikiano unaohitajika ili waweze kuishi kwa usalama na ustawi.
Amesema bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuondoa vitendo vya unyanyapaa, ukatili na kunyimwa haki vinavyoweza kuwaathiri wajane, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kushiriki katika kuwalinda na kuwawezesha kiuchumi na kijamii.
Maadhimisho ya siku ya wajane Duniani katika Halmashauri ya Mji wa Babati yataadhimishwa katika eneo la Bonga ambapo wananchi watapatiwa elimu mbalimbali kuhusu masuala ya wajane na umuhimu wa kutetea haki zao katika jamii.