FM Manyara
FM Manyara
21 July 2026, 5:04 pm

Wanariadha chipukizi mkoani Manyara pamoja na wanariadha waliowahi na wanaoendelea kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya riadha, wameahidi kuunga mkono mbio za hisani za Manyara Tanzanite Marathon zenye kaulimbiu ya “Hatua Moja, Okoa Maisha ya Mtoto”, zinazotarajiwa kufanyika Agosti 22, 2026 katika mji wa Babati.
Na Mzidalfa Zaid
Akizungumza baada ya kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath John Stephen Akhwari, amesema atahakikisha anawahamasisha wanariadha mashuhuri nchini kushiriki katika mbio hizo ili kuchangia kufanikisha lengo la kuboresha huduma za watoto wachanga, sambamba na kuibua vipaji vipya vya riadha mkoani Manyara.
Amesema mbio hizo zitakuwa fursa muhimu ya kuendeleza mchezo wa riadha nchini, kuhamasisha vijana kushiriki michezo, pamoja na kuitangaza Manyara kupitia mashindano ya kimataifa ya mbio za marathon.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ametoa wito kwa wananchi, Taasisi na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki na kuchangia mbio hizo, akisisitiza kuwa fedha zitakazopatikana zitaelekezwa katika kuboresha huduma za watoto wachanga na kuimarisha sekta ya afya mkoani humo.

Naye mwanariadha wa kimataifa Gabriel Geay amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa kuendelea kuunga mkono na kuhamasisha maendeleo ya mchezo wa riadha kwani hatua hiyo itasaidia kuongeza motisha kwa wanariadha, kuibua vipaji vipya na kuwapa vijana nafasi ya kufikia mafanikio kupitia michezo.
Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara Andrew Method amesema lengo la kwanza ni kukusanya fedha zitakazosaidia kununua vifaa tiba vya msingi vya watoto wachanga, pamoja na watoto njiti.

Mbio za Manyara Tanzanite Marathon zinatarajiwa kukutanisha washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi, huku zikiwa na lengo la kuchangisha fedha za kuboresha huduma za watoto wachanga chini ya kaulimbiu ya “Hatua Moja, Okoa Maisha ya Mtoto.”

