FM Manyara
FM Manyara
18 September 2026, 10:37 pm

Imeelezwa kuwa wananchi wengi wanakabiliwa na matatizo ya uoni hafifu na usikivu duni, hali inayochangiwa na ukosefu wa elimu sahihi kuhusu afya.
Na Marino Kawishe
Imebainika kuwa idadi kubwa ya wananchi waliofika kwenye uchunguzi wa afya katika kambi ya matibabu inayoratibiwa na Shirika la So They Can Tanzania wanakabiliwa na matatizo ya uoni hafifu na usikivu duni, hali inayochangiwa na ukosefu wa elimu sahihi kuhusu afya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na FM Manyara, Mratibu wa Idara ya Macho kutoka Hospitali ya Wilaya ya Babati, Dkt. Silvia Nyange, pamoja na Mtaalamu wa Uchunguzi wa Masikio na Macho kwa Watoto kutoka Chuo cha Elimu Maalum Patandi, Xavery Haule, wameeleza sababu mbalimbali zinazochangia hali hiyo, huku wakisema wagonjwa wengi hawafanyi uchunguzi wa afya mara kwa mara kutokana na kukosa elimu sahihi ya afya.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Masikio kutoka Chuo cha Elimu Maalum Patandi kilichopo Arusha, Xavery Haule, amesema katika kambi hiyo wameweza kuwafanyia uchunguzi wananchi na watoto na kubaini kuwa baadhi yao walikuwa na wadudu, wakiwemo mende na nyuki, ndani ya masikio, pamoja na matatizo mengine yanayoweza kusababisha usikivu hafifu.
Kambi hiyo ya matibabu inatarajiwa kufikia tamati Septemba 19, ikiwa imefanikiwa kutoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi waliojitokeza, kupitia wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Wilaya ya Babati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Kumalizika kwa kambi hiyo kunatarajiwa kuwa sehemu ya maandalizi ya kambi nyingine ya matibabu inayotarajiwa kufanyika mwaka 2027.
