FM Manyara
FM Manyara
16 September 2026, 2:06 pm

Aliyekuwa Kaimu Afisa Mtendaji na Mwenyekiti wa Kijiji Waranga Wafikishwa Mahakamani kwa Makosa ya Rushwa
Na Mzidalfa Zaid
Katika Mahakama ya Wilaya ya Hanang’ limefunguliwa shauri la uhujumu uchumi namba 20806/2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Hanang’, Mh. Arnold Kileo, dhidi ya aliyekuwa Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Waranga wilayani Hanang’, Amani Gabriel Mao, na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Abdallah Hassan Hincha.
Shauri hilo limefunguliwa Septemba 15, 2026 ambapo Kwa pamoja, washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano, yakiwemo kosa la ufujaji na ubadhirifu k/f cha 28(1) na matumizi mabaya ya mamlaka k/f cha 31, yote chini ya PCCA (Sura ya 329).
Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Wilaya ya Hanang’, Daudi Kingazi, ameieleza Mahakama kuwa mwaka 2020, washtakiwa hao kwa pamoja walighushi muhtasari wa kikao cha Halmashauri ya Kijiji cha Waranga na kufanikiwa kutoa kiasi cha shilingi 3,300,000 kutoka katika akaunti ya benki ya kijiji hicho.
Fedha hizo zilikuwa zitumike kwa ajili ya mradi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi Waranga.
Washtakiwa hao wamesomewa hati ya mashtaka na kwa pamoja wamekana kutenda makosa hayo.
Washtakiwa wametimiza masharti ya dhamana kwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili, barua ya utambulisho kutoka Serikali za Mitaa, pamoja na kusaini bondi ya shilingi 2,000,000 kila mmoja, na kwa sasa wapo nje kwa dhamana.
Shauri limeahirishwa hadi Oktoba 6, 2026, kwa ajili ya kusomwa hoja za awali (PH).