FM Manyara
FM Manyara
29 May 2026, 1:27 pm

Wananchi wa wilaya ya Hanang mkoani Manyara wameendelea kunufaika na huduma za maji safi, vyoo bora pamoja na elimu ya usafi wa mazingira na usafi binafsi baada ya shirika la WaterAid Tanzania kukabidhi rasmi mradi wa WASH katika shule ya Gidamula kwa serikali.
Na Mzidalfa Zaid
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo katika shule hiyo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semidu aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Programu wa WaterAid Tanzania, Beda Levira ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa shirika hilo Anna Mzinga, amesema mradi huo utasaidia wanafunzi pamoja na jamii ya eneo hilo waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama.
Amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kuanzisha na kuendeleza miradi ya maji kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kuboresha afya pamoja na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, mgeni rasmi Michael Semidu amelipongeza shirika la WaterAid Tanzania kwa kuendelea kuwa msaada mkubwa kwa serikali katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii, hususan sekta ya maji, afya na usafi wa mazingira.
Amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo wanaojitokeza kusaidia jamii, huku akiwataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuwanufaisha kizazi cha sasa na kijacho.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wameishukuru WaterAid Tanzania kwa kuwajengea vyoo bora pamoja na kuwapatia huduma ya maji safi na salama, huku wanafunzi wa kike wakieleza kufurahishwa na uwepo wa mazingira rafiki ya hedhi salama.
Wamesema kupitia mradi huo wamejengewa chumba maalumu cha kubadilishia pedi, vyoo bora pamoja na shimo la kutupia pedi jambo ambalo litawasaidia kujisitiri na kuendelea na masomo bila changamoto kipindi cha hedhi.
Kwa upande wao, wananchi wa eneo hilo wamesema kwa muda mrefu walikuwa wakiteseka kutokana na ukosefu wa maji na kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo, huku wakilishukuru shirika la WaterAid Tanzania kwa kufikisha huduma ya maji kijijini hapo.
Hafla hiyo pia imekwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani, ambapo vifaa mbalimbali vya usafi pamoja na miundombinu ya hedhi salama vimekabidhiwa kwa shule hiyo.
