FM Manyara
FM Manyara
18 August 2026, 3:21 pm

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara inatarajia kuwa na kambi ya madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kuanzia Agosti 19 hadi 23, 2026.
Na Mzidalfa Zaid
Akizungumza na Fm Manyara kuhusu kambi hiyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara,Robert Tarimo, amesema kambi hiyo inalenga kuwahudumia wananchi wote watakaofika hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
Tarimo amesema wananchi watapata fursa ya kupimwa na kubaini kama wana changamoto za kiafya zinazohusiana na moyo, na wale watakaobainika kuwa na matatizo wataanza kupata matibabu kulingana na hali zao.
Kwa upande wake, Daktari wa Idara ya Magonjwa ya Ndani kutoka hospital ya rufaa mkoa wa Manyara Amiri Hassan, amesema katika kambi hiyo pia kutakuwa na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto, hivyo kuwapa nafasi watoto wenye changamoto za moyo kupata uchunguzi na matibabu kutoka kwa wataalamu hao.
Ametaja baadhi ya dalili zinazoweza kuashiria uwepo wa matatizo ya moyo kuwa ni kushindwa kupumua au kuhema kwa shida, tumbo kuvimba, maumivu ya kichwa, kifua kubana, pamoja na dalili nyingine zinazohusiana na changamoto za moyo.