FM Manyara

TRA Manyara kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia

10 September 2026, 12:01 am

Picha ya baadhi ya wafanyakazi wa TRA Manyara wakipata elimu ya nishati safi ya kupikia

Wafanyakazi 23 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Manyara wamepatiwa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia umeme, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuunga mkono Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.

Na Mzidalfa Zaid

Elimu hiyo imetolewa  na Maafisa wa Mahusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Manyara waliotembelea Ofisi za TRA Manyara, ambapo wafanyakazi wameelekezwa kuhusu matumizi sahihi ya umeme katika kupikia pamoja na faida za kutumia nishati hiyo.

Akitoa elimu hiyo, Afisa Mahusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Manyara, Samuel Mandari, amesema matumizi ya umeme katika kupikia yana mchango mkubwa katika utunzaji wa mazingira, huku yakisaidia kuokoa muda na gharama za nishati.

Mandari amesema matumizi ya umeme kwa kupikia yanaweza kufikia takribani unit moja hadi mbili kwa siku, huku unit moja ikiwa na gharama ya shilingi 356, hivyo wananchi wanaweza kutumia umeme kwa ufanisi bila kuwa na hofu ya gharama kubwa.

Aidha, amewataka wafanyakazi hao kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi katika jamii kwa kuwaelimisha wananchi na kuondoa dhana kwamba kupikia kwa umeme ni gharama kubwa.

Amesema majiko ya kisasa, ikiwemo jiko janja, yameundwa kwa teknolojia inayowezesha matumizi madogo ya umeme na ni rahisi kutumia.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Manyara, Thomas Masese, ameishukuru TANESCO kwa kuwapatia elimu hiyo, akisema imewajengea uelewa utakaowawezesha kufikisha ujumbe wa matumizi ya nishati safi kwa wananchi wengine.

Amesema TRA Manyara imeamua kuanza kutumia umeme katika kupikia ofisini, huku baadhi ya wafanyakazi wakijitokeza kununua majiko ya umeme kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Kampeni ya “Pika Kijanja, Pika kwa Umeme” inayoendelea mkoani Manyara ni sehemu ya jitihada za TANESCO za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za kutumia umeme katika shughuli za kupikia.

Picha ya watumishi wa TANESCO wakitoa elimu ya nishati safi ya kupikia