FM Manyara
FM Manyara
18 September 2026, 1:46 pm

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Manyara limetoa elimu ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi wa halmashauri ya mji wa Babati.
Na Mzidalfa Zaid
Watumishi wa Halmashauri ya Mji Babati mkoani Manyara wamepewa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati isiyochafua mazingira na inayolinda afya za watumiaji.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Samuel Mandari, amesema matumizi ya nishati safi yana faida mbalimbali, ikiwemo kuokoa muda na gharama, kutunza mazingira na kulinda afya za wananchi kwa kupunguza hatari ya magonjwa yanayohusiana na mfumo wa hewa.

Amesema wananchi wanapaswa kuhamasishwa kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo umeme, gesi na mkaa mbadala, kutokana na upatikanaji wake pamoja na mchango wake katika kulinda afya na mazingira.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Aidha, wananchi wametakiwa kuendelea kubadili matumizi kutoka nishati zinazochafua mazingira na kutumia nishati safi na salama, hatua ambayo itasaidia kufikia azma ya Serikali ya kuongeza matumizi ya nishati safi nchini.
