FM Manyara
FM Manyara
1 August 2026, 11:34 pm

Wanafunzi wa Deira English Medium School wametembelea hifadhi ya Taifa Tarangire , ambapo wamepata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vya utalii na kujifunza kwa vitendo kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.
Na Mzidalfa Zaid
Mkurugenzi wa Deira English Medium School, Nada Shauri, amesema ziara hizo ni sehemu muhimu ya mchakato wa kujifunza kwani huwapa wanafunzi maarifa ya vitendo yanayoongeza uelewa wao darasani, huku zikiwajengea moyo wa kuthamini na kulinda rasilimali za asili za nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Bosco Godfrey, amesema shule imekuwa na utaratibu wa kuwaandalia wanafunzi ziara za kielimu katika hifadhi mbalimbali ili kuwawezesha kujifunza kwa vitendo, kukuza uwezo wa kufikiri kwa kina na kupanua upeo wao wa maarifa nje ya mazingira ya darasani.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki katika ziara hiyo wamesema wamefurahia kushuhudia kwa karibu wanyamapori na vivutio vingine vya asili walivyokuwa wakivisoma darasani.
Wameushukuru uongozi wa shule kwa kuendelea kuwaandalia ziara zinazowapa uzoefu halisi wa kujifunza na kuwajengea ari ya kutunza mazingira na maliasili.
Ziara hiyo ni sehemu ya dhamira ya Deira English Medium School ya kutoa elimu bora inayochanganya nadharia na vitendo, hatua inayochangia kuwajenga wanafunzi wenye maarifa mapana, ubunifu na uzalendo katika kulinda urithi wa taifa.
