FM Manyara
FM Manyara
1 June 2026, 4:00 pm

Waumini wa Kanisa la Mungu Tanzania lenye makao makuu yake mjini Babati mkoani Manyara wameiomba Serikali kuingilia kati na kusaidia kutatua mgogoro unaodaiwa kudumu kwa miaka zaidi ya minne ndani ya kanisa hilo, wakidai unasababishwa na baadhi ya viongozi kukiuka katiba ya kanisa, kutumia vibaya madaraka pamoja na fedha za kanisa.
Na mwandishi wetu
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Kamati ya katiba na Sheria ya kanisa hilo, Mwanasheria Sulle Joseph, alisema waumini wamewasilisha malalamiko yao katika ngazi mbalimbali kwa muda mrefu, lakini hadi sasa hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kutatua changamoto hizo.
Ametoa muda wa mwezi mmoja kwa viongozi wanaotuhumiwa kujiuzuru ili kupisha kufanyika kwa mkutano mkuu wa haki utakaowezesha uchaguzi wa viongozi wapya na kutaka kufanyika kwa ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za kanisa.
Amesema iwapo hatua hizo hazitachukuliwa ndani ya muda huo, waumini watalazimika kusitisha shughuli zote za kanisa kwa kufunga geti la makao makuu ya kanisa hilo.
Kwa upande wake, muumini wa kanisa hilo, James Haluu, amesema mgogoro huo umeendelea kwa zaidi ya miaka minne na umeathiri ustawi wa kanisa pamoja na umoja wa waumini.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Mkutano wa Kanisa la Mungu Tanzania, Laurent Dai, amesema wameamua kuzungumza hadharani kutokana na kile alichodai kuwa viongozi wa kanisa wameshindwa kufanya maamuzi sahihi ndani ya vikao vya maamuzi.

Kufuatia malalamiko hayo, Askofu wa kanisa la Mungu Tanzania Stephania Sanka , amakanusha tuhuma hizo na kusema wamekuwa wakisoma mapato na matumizi na wanatarajia kufanya mkutano mkuu June 5 mwaka huu.