FM Manyara
FM Manyara
30 July 2026, 5:56 pm

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amesema ushirikiano wa wadau mbalimbali ni muhimu katika kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Na Mzidalfa Zaid
RC Sendiga ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na watetezi wa haki za mazingira iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambapo ripoti hiyo inalenga kuimarisha ulinzi wa watetezi wa haki za mazingira na kuongeza ushiriki wa wananchi katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi, asasi za kiraia na wananchi ili kuhakikisha watetezi wa haki za mazingira wanapata mazingira salama ya kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa LHRC, Fundikira Wazambi, amesema lengo la mradi huo ni kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika wilaya za Kiteto na Hanang’ mkoani Manyara.
Amesema utafiti uliofanyika umebaini kuwa bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu haki za kiraia zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu mazingira, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ubora wa Programu na Kujifunza wa LHRC, Neema Sendewe, amesema ripoti hiyo imezinduliwa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuhakikisha watetezi wa haki za mazingira wanatambuliwa, wanalindwa na kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao kwa usalama.
Baadhi ya watetezi wa mazingira walioshiriki katika uzinduzi huo wamesema kila mwananchi ana wajibu wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Pia wamepongeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa kuahidi ushirikiano wa Serikali katika kuendeleza juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
