FM Manyara
FM Manyara
5 June 2026, 6:28 pm

Wananchi mkoani Manyara wamehimizwa kuhakikisha wanakagua mifumo ya umeme katika nyumba, Taasisi na maeneo ya biashara mara kwa mara ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kuzifanyia marekebisho kwa wakati.
Na Mzidalfa Zaid
Wito huo umetolewa na Afisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Manyara, Samweli Mandar, alipokuwa akizungumza kuhusu umuhimu wa matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu ya umeme kwa watumiaji.
Amesema baadhi ya hitilafu za umeme zinazotokea majumbani na kwenye maeneo ya biashara husababishwa na mifumo chakavu ya nyaya, swichi, soketi na vifaa vingine vya umeme ambavyo huendelea kutumika kwa muda mrefu bila kufanyiwa ukaguzi.
Aidha, amewashauri wananchi kutumia mafundi wenye sifa na wanaotambulika wakati wa kufunga au kufanya marekebisho ya mifumo ya umeme ili kuhakikisha kazi hizo zinafanyika kwa viwango vinavyokubalika na salama.