FM Manyara
FM Manyara
28 July 2026, 8:15 pm

Hospitali ya Mji wa Babati mkoani Manyara imepokea mitambo ya kisasa ya mfumo wa kuzalisha oksijeni tiba (Oxygen Generation System) kutoka Shirika la FREO2 Foundation, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga na wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa upumuaji.
Na Mzidalfa Zaid
Mkurugenzi wa FREO2 Foundation Maire Ruane, amesema shirika hilo linaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha huduma ya oksijeni tiba inapatikana kwa uhakika katika hospitali na vituo vya afya nchini.
Amesema kwa mwaka huu shirika hilo linatarajia kuwafikia watoto zaidi ya laki tano nchini kote, huku mkoa wa Manyara ukitarajiwa kunufaisha watoto zaidi ya elfu ishirini watakaopata huduma ya oksijeni yenye ubora na kwa wakati.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Andrew Method, amesema mitambo hiyo tayari imeanza kuleta matokeo chanya katika Hospitali ya Mji wa Babati, ambapo ndani ya mwezi mmoja imechangia kuokoa maisha ya watoto wachanga 33.
Ameeleza kuwa kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo huo, hospitali ilikuwa ikishuhudia wastani wa vifo vya watoto wachanga 80 kwa mwezi, lakini idadi hiyo imepungua hadi 50 kwa mwezi, huku lengo likiwa kufikia vifo sifuri.
Naye Mratibu Msaidizi wa Huduma za Mama na Mtoto kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mary Shadrack, amezielekeza hospitali na vituo vya afya nchini kuhakikisha vinafunga mifumo ya kuzalisha oksijeni tiba ili kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vinavyotokana na ukosefu wa oksijeni.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Babati, Dkt. Nicomedi Sammay, amesema mfumo huo umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, hususan kwa watoto wachanga na wagonjwa wanaohitaji oksijeni kwa haraka, jambo ambalo limeimarisha ubora wa huduma zinazotolewa hospitalini.
