FM Manyara
FM Manyara
26 September 2026, 9:25 pm

Kutokana na juhudi zinazofanywa na shule ya Deira English medium school katika taaluma , Serikali wilayani Babati mkoani Manyara imeupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kuwa shule ya kwanza kitaaluma katika mitihani mbalimbali ya kitaifa.
Na Mzidalfa Zaid
Serikali wilayani Babati mkoani Manyara imepongeza uongozi wa Deira English Medium School kwa kazi kubwa inayofanya katika kuhakikisha shule hiyo inafanya vizuri kitaaluma na kushika nafasi za juu katika Mkoa wa Manyara.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Thobias Abwaro, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya wanafunzi wa Darasa la Saba yaliyofanyika shuleni hapo kwa niaba ya kaimu mkuu wa wilaya ya Babati Remidius Mwema.

Kwa upande wake Mkuu wa Deira English Medium School Bosco Godfrey, amesema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri si katika taaluma pekee, bali pia katika uwekezaji wa miundombinu na huduma mbalimbali, ikiwemo usafiri wa wanafunzi kwa kutumia magari bora.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa Darasa la Saba msoma risala amesema Deira English Medium School imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma na kushika nafasi za juu katika mashindano ya kitaaluma kwa ngazi ya Mkoa wa Manyara.
Mahafali hayo yaliambatana na matukio mbalimbali yaliyowavutia wazazi, walezi na wageni, likiwemo tukio la wanafunzi wa Deira English Medium School kuwasilisha taarifa ya habari, wakionyesha uwezo wao katika uandishi na usomaji wa habari.
Aidha, mgeni rasmi Thobias Abwaro, amesema Serikali itafanyia kazi changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na uongozi wa shule hiyo, ikiwemo changamoto ya barabara inayoelekea shuleni, ili kuwezesha mazingira bora kwa wanafunzi na jamii inayozunguka shule hiyo.
