FM Manyara
FM Manyara
27 October 2026, 10:28 pm

Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kutoa elimu ya uraia na utawala bora kwa viongozi na watendaji katika wilaya ya Babati mkoani Manyara, kupitia mafunzo yaliyowakutanisha watendaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Babati na Halmashauri ya Mji wa Babati.
Na Mzidalfa Zaid
Watendaji wa vijiji , kata na halmashauri wilayani Babati mkoani Manyara wamepatiwa mafunzo ya uraia na utawala bora kwa Lengo la kuongeza uwajibikaji katika kushughulikia kero za wananchi.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji, Jane Lyimo, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha viongozi na watendaji hao kuimarisha uelewa wao kuhusu namna ya kuwaelimisha wananchi juu ya haki na wajibu wao pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria.

Lyimo amesema anaamini kuwa mafunzo hayo yatasaidia kupunguza migogoro ya ardhi inayoripotiwa katika mkoa wa Manyara, kwa kuwajengea watendaji uwezo wa kushughulikia malalamiko ya wananchi katika maeneo yao badala ya kuyaacha hadi kufikishwa katika mamlaka za juu.
Baadhi ya watendaji wa vijiji vya Sarame, Kiru Dick na Sangara, wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kuwaongoza wananchi, hususani katika kutatua migogoro ya kifamilia na migogoro ya ardhi.
Aidha, wameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kutoa mafunzo hayo, wakieleza kuwa yamewajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.

Aidha , mkuu wa wilaya ya Babati Hashim Mgandilwa amefunga rasmi mafunzo hayo katika wilaya ya Babati ambapo amewapongeza Wakufunzi kwa Mada zilizotolewa katika Mafunzo hayo na amesisitiza kuzingatia mafunzo hayo katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Mafunzo hayo yanaendelea katika wilaya zote za mkoa wa Manyara ambapo Kila wilaya itafikiwa na wataalam hao