FM Manyara
FM Manyara
3 October 2026, 8:54 am

Kufuatia kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika Shule ya Msingi Loiborsiret wilaya Simanjiro mkoani Manyara Mdau wa maendeleo Taiko Kulunju ametoa msaada wa mashine ya kuchapisha mitihani
Na Mzidalfa Zaid
Mdau wa maendeleo Taiko Kulunju ametoa msaada wa mashine ya kuchapisha mitihani yenye thamani ya shilingi milioni mbili laki nane na elfu tisini kwa Shule ya Msingi Loiborsiret, iliyopo Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, ikiwa ni hatua ya kusaidia kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji shuleni hapo.
Msaada huo umetolewa baada ya shule hiyo kukabiliwa kwa muda mrefu na changamoto ya ukosefu wa mashine ya kuchapisha mitihani tangu kuanzishwa kwake, hali iliyokuwa ikilazimu shule kupata huduma hiyo kwa njia nyingine na kuwa kero kwa walimu pamoja na wazazi.
Akizungumza wakati wa Mahafali ya 43 ya Darasa la Saba katika shule hiyo, Taiko Kulunju amesema ameamua kutoa mashine hiyo ili kusaidia shule kupunguza changamoto ya uchapishaji wa mitihani na nyaraka mbalimbali za kielimu, huku akisisitiza umuhimu wa wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha elimu.Kwa upande mwingine, walimu wa Shule ya Msingi Loiborsiret wametoa kilio chao kwa Serikali kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo, wakieleza kuwa baadhi ya changamoto hizo zinaathiri mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi.
Aidha, wazazi wameiomba Serikali kuendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wazazi na walezi wanaowazuia watoto kwenda shule, hasa katika baadhi ya familia za jamii ya wafugaji, ambapo baadhi ya watoto hupewa jukumu la kuchunga mifugo badala ya kuhudhuria masomo.
Wazazi hao wamesema ni muhimu kuwepo kwa sheria na usimamizi madhubuti ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya elimu na kwamba jukumu la watoto la kwenda shule halizuiwi kwa sababu ya shughuli za kifamilia.