FM Manyara
FM Manyara
24 August 2026, 10:17 pm

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Kampasi ya Babati mkoani Manyara kimezindua programu mbili mpya za shahada ambazo zitaanza kutolewa katika kampasi hiyo kuanzia mwaka wa masomo 2026/2027.
Na Mzidalfa Zaid
Programu hizo ni Shahada ya Uhasibu na Teknolojia ya Habari (Bachelor Degree in Accountancy with IT) pamoja na Shahada ya Sayansi ya Kompyuta (Bachelor Degree in Computer Science).
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa programu hizo, Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, amesema kuanzishwa kwa programu hizo ni hatua muhimu katika kuwaandaa vijana wenye ujuzi unaoendana na maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
Sillo amesema dunia inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, hivyo Tanzania inahitaji wataalamu wenye uwezo wa kutumia teknolojia zilizopo, kubuni mifumo mipya na kutumia maarifa kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Amesema uwekezaji katika elimu bora, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni muhimu katika kujenga rasilimali watu itakayoweza kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa kisasa na wa kidijitali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema chuo hicho kinaendelea kupanua huduma za elimu ya juu katika maeneo mbalimbali nchini, huku Kampasi ya Babati ikiwa miongoni mwa kampasi zinazokua kwa kasi.
Prof. Sedoyeka amesema IAA kwa sasa ina kampasi saba zilizopo Arusha, Babati, Bukombe, Dar es Salaam, Dodoma, Songea na Zanzibar, huku chuo hicho kikiwa na jumla ya programu 81 katika ngazi mbalimbali za elimu.
Prof. Sedoyeka amesema kuanzishwa kwa programu za shahada katika Kampasi ya Babati ni sehemu ya mkakati wa kuongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wa Manyara na maeneo mengine ya Tanzania.
Amesema chuo kinaendelea pia kuimarisha mitaala yake ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na kutoa elimu inayowawezesha wahitimu kujiajiri na kuajiriwa.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa IAA Kampasi ya Babati wameeleza kuwa wanapata elimu bora inayowawezesha kupata maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira. Wamesema walimu na wakufunzi chuoni hapo wanawasaidia kuelewa masomo yao na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za kiutendaji baada ya kuhitimu.
Wanafunzi hao wameeleza kuwa kuanzishwa kwa programu za shahada katika Kampasi ya Babati kutawasaidia vijana wengi kupata elimu ya juu bila kulazimika kusafiri kwenda mbali na maeneo yao.
Uzinduzi wa programu hizo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuongeza fursa za elimu ya juu mkoani Manyara, pamoja na kuandaa wataalamu watakaoweza kushiriki katika maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na uchumi wa kidijitali.
