FM Manyara

DC Kaganda aamuru wananchi waliojenga eneo la mwekezaji kuhama

24 April 2026, 2:02 pm

Picha ya Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Emmanuela Mtatikolo Kaganda

Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Emmanuela Mtatikolo Kaganda amewataka Wananchi wa Vijiji vya Kiru, Masware na Marangi waliojenga makazi yao ndani ya eneo la muwekezaji kubomoa nyumba zao na kuacha eneo hilo likiwa wazi kwani eneo hilo sio lao Kisheria, hivyo watoke katika maeneo hayo ili kuondoa mgogoro uliopo kati ya ya Muwekezaji (Dudumela Plantation) na Wananchi wa Vijiji hivyo.

Na Mzidalfa Zaid

Ametoa maelekezo hayo mara baada ya kufika katika vijiji hivyo vyenye mgogoro wa Ardhi na muwekezaji “Dudumela Plantation” Kwa Muda Mrefu huku akiwataka Wananchi hao waliovamia kwenda kujenga sehemu iliyotengwa rasmi Kwa ajili yao.

DC Kaganda amewataka wananchi waishi kwa utulivu katika eneo lililoombwa kwa ajili ya wananchi waliovamia eneo hilo la muwekezaji ili kuondoa ugomvi uliopo kati ya muwekezaji na Wananchi wa Vijiji hivyo. Amesisitiza uwepo wa amani katika maeneo hayo ili shughuli mbalimbali za kimaendeleo ziendelee.

Pia, amewaagiza wataalamu wa ardhi kutoka Halmashauri zote mbili (Halmashauri ya Babati Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Babati) kuwapitisha wananchi upya katika mipaka ya maeneo hayo ili wananchi waelewe mipaka ya maeneo hayo kwani itawasaidia kuhepusha Migogoro mingine kutokea katika eneo hilo, huku akimshauri muwekezaji kuendeleza maeneo ambayo yapo karibu na mipaka ya eneo hilo ikiwemo kupanda miti.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Babati SSP Ernesta Mwambinga amewaomba Wananchi kusimamia maeneo hayo yaliyoombwa Kwa ajili yao huku akiwataka kwenye viongozi wa serikali ya kijiji kusimamia maeneo hayo vinginevyo Sheria zitachukuliwa dhidi yao.