FM Manyara
FM Manyara
1 August 2026, 11:53 pm

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kaskazini imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kulinda afya za wananchi na mazingira.
Na Mzidalfa Zaid
Akizungumza na FM Manyara, Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, George Mhina, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia husaidia kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa kuni na mkaa, huku yakichangia pia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti.
Mhina amewahimiza wananchi kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia kwa kuwa ni salama, yenye ufanisi na inayorahisisha shughuli za kila siku za kupika.
Kwa upande wake, Afisa Huduma kwa Wateja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Bahati Bakunda, amesema wananchi wenye maswali au wanaohitaji ufafanuzi kuhusu huduma za nishati na maji wanaweza kuwasiliana na EWURA kupitia namba ya simu ya bure ili kupata huduma na maelezo kutoka kwa wataalamu wa mamlaka hiyo.
Amesema EWURA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha wanafahamu haki zao, wajibu wao na namna bora ya kutumia huduma za nishati na maji kwa usalama na ufanisi.