FM Manyara

RC Shigela awataka wananchi kushiriki kampeni ya ushirika Manyara

30 September 2026, 9:17 pm

Picha ya mkuu wa mkoa wa Manyara Martin Shigela

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martin Shigela, amewataka wananchi mkoani humo kutumia fursa ya kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” kueleza changamoto zinazowakabili wanaushirika ili ziweze kufanyiwa kazi na kupata ufumbuzi.

Na Mzidalfa Zaid

Mkuu wa mkoa wa Manyara Martin Shigela amepongeza tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulinda ushirika ambapo amewataka wananchi kutumia uwepo wa kampeini hiyo kujifunza masuala mbalimbali ya ushirika.

Shigela ameyasema hayo baada ya kupokea ugeni wa viongozi kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) waliomtembelea ofisini kwake, ambao wanaendelea na kampeni hiyo inayolenga kuhamasisha uadilifu na kulinda maslahi ya wanachama wa vyama vya ushirika.

Sauti ya Mkuu wa mkoa wa Manyara Martin Shigela

Awali Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania (TCDC), Consolata Kiluma, wakati wa ufunguzi wa kliniki ya ushirika mkoani Manyara, iliyofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani kuanzia Septemba 30 hadi Oktoba 2, 2026, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kueleza kero zao na kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya ushirika.

Sauti ya Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania (TCDC), Consolata Kiluma

Amesema kliniki hiyo inalenga kusikiliza na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wanaushirika, huku ikitoa elimu kuhusu umuhimu wa uadilifu katika usimamizi na uendeshaji wa vyama vya ushirika.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Rift Valley Cooperative Union (RIVACU), Yuda Sulle, amesema kampeni hiyo ni muhimu katika kuimarisha uadilifu, uwajibikaji na usimamizi wa vyama vya ushirika kwa manufaa ya wanachama wake

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wakulima wa Miwa Mkoa wa Manyara, Omari Mazende, ameishukuru TCDC kwa kuanzisha kliniki hiyo mkoani humo, akieleza matumaini yake kuwa itasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima wa miwa na vyama vyao vya ushirika.

Sauti ya Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wakulima wa Miwa Mkoa wa Manyara, Omari Mazende,