FM Manyara

Wakulima 105 wapata mafunzo matumizi sahihi ya mbolea

26 October 2026, 9:16 pm

Picha ya Meneja wa TFRA Kanda ya kaskazini akitoa elimu kwa wakulima

Wadau 105 wa sekta ya kilimo kutoka halmashauri 11 za mikoa ya Singida, Morogoro na Manyara wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea.

Na Mzidalfa Zaid

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kaskazini, kwa kushirikiana na shirika la Farm Africa, wametoa mafunzo kwa wakulima, wafanyabiashara wa mbolea na wakulima vinara kutoka halmashauri 11 za mikoa ya Manyara, Singida na Morogoro, kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija katika kilimo.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe, amesema jumla ya wakulima na wafanyabiashara wa pembejeo 105 wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea.

Sauti ya Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe

Liampawe amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa washiriki kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, hatua inayotarajiwa kuwasaidia kuboresha uzalishaji na kuongeza tija katika shughuli za kilimo.

Kwa upande wake, Afisa Mradi kutoka shirika la Farm Africa, Stoney Lengai, amesema shirika hilo limewezesha mafunzo hayo ili kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi kuhusu matumizi ya mbolea na kuweza kuitumia kwa ufanisi katika shughuli zao za kilimo.

Sauti ya Afisa Mradi kutoka shirika la Farm Africa, Stoney Lengai,

Nao baadhi ya wakulima kutoka mikoa ya Manyara, Singida na Morogoro wameishukuru TFRA pamoja na Farm Africa kwa kutoa mafunzo hayo, wakieleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo na kuongeza tija katika uzalishaji.Kichwa cha habari.

Sauti ya wakulima

Kupitia mafunzo hayo, wadau wamepata fursa ya kuimarisha uelewa wao kuhusu umuhimu wa kutumia mbolea kwa kuzingatia mahitaji ya zao, hali ya udongo na kanuni bora za kilimo.

Aidha, ushiriki wa wafanyabiashara wa mbolea,wakulima vinara, na viongozi wa AMCOS unatarajiwa kusaidia kueneza maarifa hayo kwa wakulima wengi zaidi katika maeneo yao.Ushirikiano kati ya TFRA na Farm Africa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, kuboresha huduma kwa wakulima na kuendeleza kilimo chenye tija na endelevu.