FM Manyara
FM Manyara
9 October 2026, 4:12 pm

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoani Manyara umetoa motisha kwa waajiri na wanachama wanaofanya vizuri katika ulipaji wa michango kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uwajibikaji na kuimarisha huduma za hifadhi ya jamii.
Leo ikiwa ni kilele Cha wiki ya huduma kwa wateja, mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii(NSSF) umeandaa hafla fupi ya kuwapongeza wanachama na waajiri ambao wamekuwa wakilipa michango yao kwa wakati.
Na Mzidalfa Zaid
Akizungumza baada ya kukabidhi vyeti vya pongezi pamoja na zawadi mbalimbali kwa washiriki waliofanya vizuri, Kaimu Meneja wa NSSF mkoa wa Manyara, Abdallah Kaporo, amesema hatua hiyo inalenga kutambua na kupongeza waajiri na wanachama wanaotekeleza wajibu wao kwa kuchangia kwa wakati.
Ameongeza kuwa waajiri wengine wanapaswa kuiga mfano huo kwa kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao mapema na kwa wakati, ili wanachama waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na mfuko huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Mbulu Winners, ambaye ni miongoni mwa waliopokea motisha hiyo, ameishukuru NSSF kwa kutambua mchango wao, akisema shule hiyo imekuwa ikitimiza wajibu wake wa kuwasilisha michango kwa wakati.
Naye mmoja wa wanachama anayejichangia mwenyewe ameushukuru mfuko huo kwa huduma zake, akieleza kuwa umekuwa na mchango katika kumsaidia kupata huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za matibabu.