FM Manyara
FM Manyara
10 September 2026, 9:17 pm

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea na shughuli za utafiti wa uwepo wa mafuta na gesi nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza fursa za upatikanaji wa nishati na kupanua wigo wa rasilimali za mafuta na gesi kwa matumizi ya sasa na baadaye.
Na Mzidalfa Zaid
Hayo yameelezwa leo Septemba 10, 2026 na wataalamu wa TPDC katika kikao kazi na waandishi wa habari mjini Babati, mkoani Manyara, kilicholenga kuwaongezea wanahabari uelewa kuhusu shughuli za shirika hilo pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika sekta ya mafuta na gesi.
Kwa mujibu wa TPDC, tafiti hizo zinaendelea katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo mikoa ya Arusha, Tabora, Simiyu na Shinyanga, huku mkoani Manyara utafiti ukiendelea katika eneo la Eyasi-Wembere. Hatua hiyo inalenga kubaini uwepo wa rasilimali za mafuta na gesi chini ya ardhi na kuweka msingi wa matumizi ya rasilimali hizo endapo zitabainika.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara anayesimamia Sekta ya Uchumi na Uzalishaji, Faraja Ngerageza, amesema tafiti hizo ni muhimu katika kuongeza uwezo wa Tanzania wa kujitegemea katika upatikanaji wa nishati.
Amesema wananchi wanaoishi katika maeneo yanayotekelezwa miradi hiyo wataendelea kunufaika kupitia programu mbalimbali za maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu, utoaji wa huduma za kijamii na kuwawezesha kupata fursa mbadala za kiuchumi.
Ngerageza pia amewataka wananchi kupuuza taarifa zisizo na uthibitisho kuhusu Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), hususan zinazodai kuwa mradi huo unasababisha uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Frances Lupokela, amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo mkoani Manyara, jumla ya wananchi 494 wameguswa na mradi, ambapo 491 wamelipwa fidia, huku wananchi watatu wakikabiliwa na changamoto za migogoro ya ardhi.

Naye Mhandisi Mwandamizi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Hassan Temba, amesema lengo la kukutana na waandishi wa habari ni kutoa elimu kuhusu kazi kubwa zinazofanywa na TPDC pamoja na kueleza mafanikio yanayotokana na uwepo wa mradi wa bomba la mafuta.

Mradi wa EACOP unaanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ukipita katika mikoa minne ya Tanzania ukiwemo mkoa wa Manyara.